Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Mike Wendling
- Nafasi, BBC
Baada ya kutangaza atakubali zawadi ya ndege kutoka Qatar, Donald Trump amekumbwa na ukosoaji mkubwa, kutoka kwa wafuasi na wakosoaji wake nchini Marekani.
Wapinzani wa Trump katika Chama cha Democratic wamemkosoa rais huyo baada ya kusema atakubali zawadi ya ndege ya kifahari kutoka kwa familia ya kifalme ya Qatar.
Lakini kinachoweza kumsumbua zaidi rais - ni kwamba baadhi ya wafuasi wake pia wana mashaka makubwa kuhusu zawadi hiyo, hata kama bado haijatolewa.
Wafuasi wake wa Maga (Make America Great Again) wamesema jambo hilo ni kama "hongo" au ufisadi wa hali ya juu ambao Trump mwenyewe amekuwa akiahidi kuutokomeza.
Familia ya kifalme ya Qatar inapanga kutoa ndege ya kifahari aina ya Boeing 747-8, inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 400 (£300m), kwa Idara ya Ulinzi ya Marekani ili itumike kama sehemu ya ndege zinazoitwa Air Force One - ndege rasmi za usafiri wa rais.
Skip Iliyosomwa zaidi and continue reading
Iliyosomwa zaidi
Kwanini Simba SC imefungwa Morocco lakini haijachapwa fainali CAF?
Tetesi za Soka Ulaya Jumapili: Rashford atapunguziwa mshahara kwa kuhama Barca
Mbivu na mbichi ya Profesa Janabi katika uchaguzi wa Mkurugenzi wa WHO Afrika
Ibrahim Traore: Habari potofu zinazotumiwa kumtukuza kiongozi huyu wa kijeshi
End of Iliyosomwa zaidi
Ndege za sasa zimekuwa zikitumika tangu 1990. Ikulu ya White House inasema ndege hiyo mpya - ambayo inaweza kuhitaji miaka na mamilioni ya dola ili kuirekebisha na kuiboresha - itapelekwa kwenye maktaba ya rais Trump mwishoni mwa muhula wake.
Kwanini Trump anazuru tena mataifa ya Ghuba?
Qatar yanunua ndege za kivita kutoka Marekani
Kwa nini mikataba mingi mikubwa ya amani inasimamiwa na Saudi Arabia na Qatar?
Wafuasi wa Trump
Mhafidhina wa Daily Wire, Ben Shapiro anasema: "Qatar haimpi Rais Trump ndege ya dola milioni 400 kwa moyo mwema," amesema. "Wanajaribu kuingiza pesa kwenye mifuko kwa mtindo wa kurubuni."
Shapiro na wahafidhina wengine wametoa madai kwamba Qatar imepeleka pesa katika vikundi vya kigaidi - madai ambayo nchi hiyo imekanusha - na kuwaita Waqatari "watetezi wakubwa wa ugaidi katika kiwango cha kimataifa."
Laura Loomer, mhafidhina mwingine katika mitandao ya kijamii na muungaji mkono wa utawala wa Trump, alikatiza mtiririko wake wa jumbe za kumuunga mkono Trump na kukosoa hatua hiyo.
Ingawa alisema bado anamuunga mkono rais, aliita zawadi hiyo ni "doa" na kuchapisha katuni ya Trojan Horse, iliyochorwa kama ndege iliyojaa wanamgambo wa Kiislamu wenye silaha.
Gazeti la New York Post, ambalo kwa kawaida husukuma ajenda za Maga, liliandika tahariri: "Ndege ya Qatar si zawadi ya bure' - na Trump hapaswi kuikubali kama ilivyo."
Naye Mark Levin, mfuasi wa rais kwenye Fox News, alichapisha maoni kwenye mtandao wa kijamii wa X akiituhumu Qatar kuwa "taifa la kigaidi" na kuandika: "Ndege yao na vitu vingine vyote wanavyonunua kutoka katika nchi yetu, havitokuwa kinga wanayoitafuta."
Wakati wa muhula wake wa kwanza, Trump mwenyewe aliishutumu Qatar kwa kufadhili makundi ya kigaidi.
Qatar na Marekani zajibu
Chanzo cha picha, Reuters
Ubalozi wa Qatar jijini Washington umeeleza kupitia mahojiano ya Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani na CNN kuwa:
"Ni suala kati ya serikali na serikali. Halina muingiliano wowote na uhusiano binafsi - si kwa upande wa Marekani, wala upande wa Qatar. Ni jambo kati ya wizara mbili za ulinzi.”
"Kwa nini tununue ushawishi nchini Marekani?" aliongeza, akisema Qatar "daima imekuwa mshirika anayetegemewa na anayeaminika. Huu sio uhusiano wa upande mmoja."
Kujibu ukosoaji wa mpango huo, Ikulu ya White House kupitia semaji wa Trump, Karoline Leavitt amesema utawala wa Trump "umejitolea kuwepo kwa uwazi kamili."
"Zawadi yoyote inayotolewa na serikali ya kigeni kikawaida inakubalika kwa kufuata kikamilifu sheria zote zinazotumika," alisema.
Katiba inasemaje?
Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa hakuna chochote ambacho Marekani itatoa kufuatia zawadi hiyo, wachambuzi wengi wanasema, itakuwa ni ujinga kutarajia kwamba familia ya kifalme ya Qatari, itatoa zawadi kubwa bila masharti yoyote.
"Kwa hakika wanaona kwamba ukimpa Donald Trump zawadi, inaweza kuwa na matokeo mazuri," anasema Doug Heye, mtaalamu wa mikakati ya kisiasa na mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano katika Kamati ya Kitaifa ya Republican.
Katiba ya Marekani inazuia maafisa kukubali "zawadi yoyote, Malipo, Ofisi, au Cheo, cha aina yoyote ile, kutoka kwa Mfalme, Mwanamfalme, au Nchi ya kigeni."
Lakini Ikulu ya Marekani imesema, ndege hiyo imetolewa zawadi kwa serikali ya Marekani.
Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Pam Bondi ameripotiwa kuchunguza uhalali wa mpango huo na kusema kwa sababu hakuna masharti ya wazi yaliyoambatanishwa, haitokuwa ni hongo.
Lakini wahafidhina na wengine wameeleza kwamba Bondi alisajiliwa kama mtetezi wa Qatar kabla ya kujiunga na baraza la mawaziri la Trump, wakati fulani akipata hadi dola 115,0000 (£87,000) kwa mwezi kutokana na kazi yake kwa serikali ya Qatar.
Shirika la Trump pia lina uhusiano na Qatar na mwezi uliopita lilitangaza mpango wa kujenga hoteli ya kifahari nchini humo.
Trump na Republican
Wakati wa mkutano na wanahabari katika Ikulu ya White House siku ya Jumanne rais alimkashifu ripota ambaye aliibua maswali kuhusu maadili ya mpango huo.
"Unasemaje kwa watu wanaoiona ndege hiyo ya kifahari kama zawadi binafsi kwako?" aliuliza mwanahabari wa ABC, Rachel Scott.
"Unapaswa kusikia aibu kuuliza swali hilo," Trump alijibu. "Wanatupa ndege ya bure," rais alisema.
Kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, rais baadaye alichapisha tena jumbe kadhaa zilizoonyesha kwamba Sanamu ya Uhuru ilikuwa zawadi kutoka Ufaransa, na aliandika siku ya Jumanne: "Boeing 747 ni zawadi kwa Jeshi la Anga la Marekani/Idara ya Ulinzi, SI KWANGU!"
"Ni MPUMBAVU pekee ndiye ambaye hatokubali zawadi hii kwa niaba ya nchi yetu," aliandika.
Hata hivyo baadhi ya watu ndani ya chama cha Republican cha Trump wameeleza wasiwasi wao.
Rand Paul, seneta wa Republican kutoka Kentucky, aliiambia Fox News, "najiuliza ikiwa uwezo wetu wa kukosoa rekodi ya haki za binadamu [ya Qatar] itafunikwa na zawadi hii kubwa.”
Seneta mwingine wa Republican, Ted Cruz wa Texas, alisema kukubali zawadi hiyo kutaleta "matatizo makubwa ya ujasusi na ufuatiliaji."
Trump alipata uungwaji mkono ndani ya chama chake. "Cha bure kizuri. Unajua hatuna pesa nyingi kwa sasa za kununua vitu kama hivyo," alisema Seneta Tommy Tuberville.
Doug Heye, mtaalamu wa mikakati wa chama cha Republican, amesema mpango huo unaweza usiathiri kuungwa mkono kwa Trump kutoka kwa wafuasi wake.
"Kwa miaka sasa Trump ameweza kuzigeuza kashfa ambazo zingeweza kuwadhoofisha wanasiasa wengine kuwa mambo ambayo tunayasahau. Ana ujuzi sana katika hilo," amesema.
Trump aisifu Saudi Arabia kwa kuitenga Qatar
Mzozo wa DRC: Ushawishi wa Qatar katika mzozo huu utafanikiwa?
Kwanini Qatar imeshindwa kuipatanisha Israel na Hamas?
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi